Rais wa Marekani anayeondoka Barack
Obama amesema huenda akazungumza, kinyume na utamaduni wa siasa
Marekani, iwapo mrithi wake Donald Trump atatishia "maadili muhimu" ya
Marekani.
Huwa desturi kwamba marais wa zamani wa Marekani huwa
hawajiingizi sana katika siasa baada ya kuondoka madarakani na huwa
hawazungumzi kuhusu warithi wao.
Akiongea katika kikao na
wanahabari wakati wa mkutano wa nchi za Asia na Pasifiki (Apec) mjini
Lima, Peru.
Lakini amesema kwamba, kama raia, huenda akalazimika kuzungumza kuhusu baadhi ya mambo.
"Ninataka kuiheshimu afisi na kumpa rais mteule fursa ya kueleza
msimamo wake na mipango yake bila mtu kujitokeza kumkosoa," Bw Obama
alisema.
Lakini akaongeza, kwamba iwapo suala "litagusa maadili
muhimu ya Marekani na imani yetu, na nafikiri kwamba inahitajika au
itafaa kwangu kutetea maadili hayo, badi nitalitathmini wakati huo".
Kisha, amejieleza kama "raia wa Marekani anayejali sana taifa".
Akiongea katika kikao cha wanahabari wakati wa kufungwa kwa mkutano
mkuu wa viongozi wa Apec, Bw Obama amesisitiza kwamba ataonyesha
utaalamu kwa kundi la Bw Trump wakati wa mpito sawa na ilivyofanyika kwa
kundi lake wakati wa kuondoka kwa mtangulizi wake George W Bush.
Bw
Bush, tangu aondoke madarakani, amejizuia kuzungumzia utawala wa Bw
Obama. "Sidhani hilo linasaidia kwa vyovyote," aliambia CNN mwaka 2013,
baada ya Obama kuchaguliwa kwa mara ya pili.
"Ni kazi ngumu. Ana
mambo mengi ya kushughulikia kwenye ajenda yake. Rais wa zamani hafai
kuyafanya mambo kuwa magumu zaidi kwake. Marais wengine wa zamani
wamechukua uamuzi tofauti; huu ni wangu."
Msimamo wa Bw Bush unafuata desturi, ambapo marais wa Marekani huwa wanajiepusha kuwakosoa watangulizi au warithi wao.
Bw Obama alisema wazi kwamba hataingilia msimamo wa Bw Trump kabla ya muhula wake kumalizika Januari mwakani.
Lakini
ufafanuzi wake kwamba, atakapokuwa raia wa kawaida, atatetea "maadili
muhimu", ameutoa huku kukiendelea kuwa na wasiwasi miongoni mwa makundi
ya kutetea haki za kiraia kuhusu watu wanaoteuliwa na Bw Trump
kushikilia nyadhifa kuu katika serikali yake.
Mwanasheria mkuu aliyeteuliwa na Bw Trump, Jess Sessions, alizuiwa
kuhudumu kama jaji wa dola mwaka 1986 kwa sababu ya kutoa matamshi ya
ubaguzi wa rangi.
Bw Obama amesema anaamini majukumu makuu ya
urais yatamlazimu Bw Trump kulegeza baadhi ya sera zake kali ambazo
alizitetea wakati wa kampeni.
'Kushindwa kwa Democratic'
Alipoulizwa
kuhusu kushindwa kwa chama cha Democratic chini ya Hillary Clinton, Bw
Obama alikosoa kampeni zilizolenga "makundi fulani", badala ya
kukumbatia taifa lote.
Bi
Clinton amekosolewa kwa kuangazia sana watu wa jamii fulani, wakiwemo
Walatino na wanawake, ambao waliaminika kumuunga mkono badala ya watu
wote.
Njia kama hiyo "haitakusaidia kushinda uungwaji mkono wa
watu wengi kama inavyohitajika," Bw Obama alisema na kuongeza kwamba
chama hicho kilihitaji "ujumbe bora zaidi".Toa
maoni yako.