Thursday, November 17, 2016

Serikali ipige marufuku viwanda feki vya pombe kali


viwanda-feki-vya-pombe-kali

 
 Toleo la gazeti Mtanzania liliripoti kuwa kiwanda feki cha kutengeneza pia konyagi feki na bidhaa zake kimegundulika Dar es Salaam baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla, kuvamia kiwanda hicho.


Kwamba tukio hilo lilitokea juzi baada ya Dk. Kigwangalla kwa kushirikiana na Maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Tume ya Ushindani pamoja na Jeshi la Polisi kunasa kiwanda hicho bubu.

Kiwanda hicho kilinaswa kwenye nyumba ya mwanamke anayejulikana kwa jina moja la Koku maarufu ‘Mama Kareem’ eneo la Sinza Kijiweni, Dar es Salaam kikitengeneza pombe feki ya konyagi, viroba na pombe kali ya smirnoff.

Katika kiwanda hicho pia kulikutwa malighafi mbalimbali zinazotumika kutengenezea bidhaa hizo, likiwamo dumu kubwa lililokuwa limejaa gongo.

Vingine ni dumu la spirit lita 20, chupa tupu na zilizojazwa kwa ajili ya kusambazwa, vizibo vya chupa za konyagi na smirnof pamoja na vifungashio vya aina mbalimbali.

Meneja wa TFDA Kanda ya Mashariki, Emmanuel Alphonce, alisema kiwanda hicho kimebainika baada ya kupata taarifa kutoka kwa majirani wa mwanamke huyo ambao walitilia shaka mwenendo wa biashara alizokuwa akizifanya.

Kwamba kilikamatwa kiwanda kinachotengeneza konyagi feki huko Sinza, na kiwanda hicho kilikuwa kinatengeneza vinywaji hivyo kwa kutumia ‘spirit’ ambayo inachanganywa na gongo.

Kwamba bidhaa zilizokamatwa ni pamoja na dumu kubwa la kuhifadhia pombe na watu wawili ambao inasemekana ni wafanyakazi wa kiwanda hicho.

Tunapenda kutoa hadhari kwamba Novemba 8, mwaka huu, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema Serikali inazishauri sekta binafsi kuanzisha viwanda vya kutengeneza gongo kwa viwango vya usalama na ubora.

Kwamba faida za gongo zinafahamika, wataalamu wake wana uwezo wa kujua faida ya kinywaji hiki ila tatizo ni usalama.

Kwamba atawaelekeza wataalamu hawa kuhakikisha kuwa kinywaji hicho kinatengenezwa kwa usalama. Waziri Mwijage aliyasema hayo bungeni hivi majuzi

Juzi mkulima wa kijiji cha Kingo, wilaya ya Kilwa mkoani Lindi alikutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake baada ya kunywa viroba vya konyagi.

Mkulima huyo anadaiwa kunywa pombe hiyo alipokuwa kwenye sherehe kijijini hapo.

Tunasema kuwa pamoja na tamko la Waziri Mwijage kuwa na nia nzuri, lakini utengenezaji wa ovyo na kumiliki viwanda feki vya kutengeneza pombe kali ni majanga ya kiafya.

Tunasisitiza kuwa ni majanga ya kiafya kwa sababu vijana wengi, wakiwamo waendesha magari na bodaboda, wanatumia vinywaji hivi feki na kusababisha ajali nyingi, mbali na kudhuru afya zao.

Tunashauri Serikali ifanye misako mingi nchi nzima kama msako uliofanywa Sinza Kijiweni na kuwakamata wenye viwanda hivi feki.

Tunadhani viwanda feki vinavyotengeneza konyagi feki na aina nyingine za pombe kali ni janga la kitaifa.

Tunasema viwanda hivi vipigwe maruku mara moja.

Toa comment zako.
 

No comments:

Post a Comment