Thursday, November 17, 2016

Waathirika tetemeko la ardhi mkoani kagera wapewa mabati, saruji





MAKUNDI ya wasiojiweza ambao ni waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera wameanza kupatiwa msaada wa mabati 20 kwa kila kaya na mifuko mitano ya ya saruji. 


Hatua hiyo imechukuliwa kwa wananchi hao katika wilaya sita za mkoa huo kwa kuanza na wazee, walemavu, wajane na watu wasiojiweza.

Mkuu wa Mkoa huo Meja Jenerali mstaafu, Saalim Kijuu alifanya uzinduzi juzi wa ugawaji wa vifaa hivyo katika ofisi ya Kata ya Kashai katika Manispaa ya Bukoba.

Alisema vifaa vya ujenzi kwa makundi hayo utafanyika katika wilaya za Muleba, Misesenyi,Karagwe, Manipaa ya Bukoba na Bukoba Vijijini.

Alisema hatua ya awali imegawa kaya 200 kati ya kaya 370 kwa kuanzia mtaa wa Rwome na Kijiji cha Ibosa katika kata ya Nyakato.

Aneth Kiiza, mkazi wa mtaa wa Rwome Kata Kashai akizungunza kwa niaba ya mama yake imelda Kiiza (95), alisema aliwashukuru viongozi kwa msaada huo.

Alisema nyumba aliyokuwa akiishi mama huyo ilianguka ukuta upande wa kulia na kushoto na walikosa maeneo ya kuishi kwa muda mrefu.

Kiiza alisema misaada aliyopewa mama yake itasaidia kupata angalau chumba kimoja cha kuishi.

Alisema mama yake hana uwezo wa kujijengea nyumba kutokana na hali yake ya uchumi kuwa duni.

Pia alisema kuwa gharama za ujenzi wa nyumba nzima ni Sh milioni 4.8, fedha ambazo hana.

Diwani wa Kata ya Kashai, Nurulhuda Kabaju (Chadema), alisema yanapotokea matatizo kama ya tetemeko la ardhi watoto wawakumbuke wazazi wao kwa kutoa misaada ya hali na mali.

Khafisa Khamis (75) mkazi wa Kijiji cha Ibosa Kata Nyakato ambaye ni mjane alisema nyumba yake ilipasuka kila kona hivyo anaishukuru serikali kwa kumpatia mifuko mitano ya saruji na mabati 20.
 
Toa comment.
 

No comments:

Post a Comment