Wakimbizi raia wa Sudan Kusini waliokimbilia nchini Uganda, wameelezea namna walivyolazimika kukimbia kuuawa kutoka kwenye mikono ya wanajeshi wa Serikali huku wakikwepa pia kuingia kwenye mikono ya wapiganaji wa waasi.
Mamia kwa maelfu ya raia wamelikimbia taifa hilo jipya kabisa duniani, toka kuzuka kwa mapigano mapya kwenye jiji kuu la nchi hiyo, Juba, mwezi Julai mwaka huu, kufuatia makabiliano ya wanajeshi wa Serikali na wale wa kiongozi wa waasi Riek Machar.
Magharibi mwa nchi hiyo kwenye mji wa Yei, sehemu ya wanajeshi wa Serikali, wanatumia mapanga kuua raia, wakiwatuhumu kuwa wanataka kujiunga na vikosi vya waasi.
"Kama wiki mbili zimepita, wanajeshi walikuja kwa kaka yangu Emmanuel usiku na kumtaka afungue mlango," alisema Abraham Aloro, kijana mwenye umri wa miaka 20 ambaye alikuwa mkulima wa tumbaku kwenye mji huo.
Mji huo ambao uko umbali wa kilometa 50 na mpaka wa nchi ya Uganda, umekuwa ni sehemu ya makabiliano kati ya vikosi vitiifu kwa Rais Salva Kiir na vile vya kiongozi wa waasi Riek Machar ambaye sasa anaishi uhamishoni.
"Walikuwa wanamtuhumu kujiunga na waasi," alisema Aloro. "Hakuwa hivyo kaka yangu lakini walimkatakata hadi kufa, tuliona mwili wake ilipofika asubuhi".
Baada ya kuhisi usalama wake nao uko hatarini, Aloro aliamua kukimbilia kwenye kambi ya wakimbizi ya Kuluba iliyoko kaskazini mwa nchi ya Uganda, kambi ambayo iko umbali wa kilometa 7 na mpaka wa Sudan Kusini.
Kwa wastani wakimbizi wanaokadiriwa kufikia 2400 wanawasili Uganda wakitokea Sudan Kusini kila siku, watu hawa wanakimbia machafuko ya kisiasa ambayo yalifuatiwa na kuvunjika kwa makubaliano ya amani kati ya rais Kiir na Machar.
Zaidi ya wakimbizi laki 3 na elfu 30 waliwasili nchini Uganda mwaka uliopita.
Katika hatua nyingine, umoja wa Mataifa umeonya kuhusu uwezekano wa nchi hiyo kukumbwa na mauaji ya kimbari na kwamba huenda hata wanajeshi wa kulinda amani walioplekwa nchini humo wakashindwa kudhibiti mapigano ikiwa yatatokea.
Umoja wa Mataifa unazitaka pande zinazohasimiana nchini Sudan Kusini kusitisha mapigano na kuhubiri amani, huku ukisisitiza umuhimu wa kupelekwa kwa kikosi maalumu cha kukabiliana na wanajeshi au waasi watakaoanzisha mapigano.
Naomba comment zako .
No comments:
Post a Comment